Rais wa Venezuela Nicolás Maduro alitoa kauli kali akisema kuwa taifa lake liko tayari kwa vita ya silaha dhidi ya Marekani endapo kutakuwa na shambulio lolote. Kauli hiyo ilitolewa katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Caracas, kufuatia ongezeko la meli za kivita za Marekani katika Bahari ya Karibiani.
Maduro alieleza kuwa Venezuela inakabiliwa na tishio kubwa zaidi la kijeshi katika historia ya kisasa ya Amerika Kusini, akitaja uwepo wa meli nane za kivita, makombora zaidi ya 1,000, na manowari ya nyuklia karibu na mipaka ya nchi yake.
“If Venezuela were attacked, we would declare an armed struggle and a Republic in arms,” alisema Maduro, akisisitiza kuwa taifa lake halitasita kujibu kwa nguvu kamili ikiwa kutakuwa na uvamizi.
Serikali ya Venezuela imeanza kuandikisha wanamgambo wa kiraia na kuimarisha ulinzi wa mipaka, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kujibu tishio lolote la kijeshi. Hatua hizi zimeibua mjadala mkubwa wa kimataifa kuhusu mvutano unaoongezeka kati ya Marekani na Venezuela.
Kwa sasa, hakuna tamko rasmi kutoka Ikulu ya Marekani kuhusu kauli ya Maduro, lakini wachambuzi wa kisiasa wanaonya kuwa hali inaweza kuchochea mzozo wa kimataifa ikiwa haitadhibitiwa kwa njia ya kidiplomasia.
by Twaha Ahmadi | Iliandikwa 07/09/2025